Kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric usiku wa kuamkia leo alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA mwaka 2017/18, na kumaliza zama za washambuliaji wawili waliotamba kwa muda mrefu Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Kiungo huyo wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid, alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa kuwabwaga  Ronaldo na Mohamed Salah, ambao walikua kwenye orodha ya tatu bora ya mwisho iliyotolewa na FIFA mwezi mmoja uliopita.

Modric anatwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza katika maisha yake na juhudi kubwa iliyombeba hadi kufikia mafanikio hayo ni uwezo na ushirikiano aliouonyesha akiwa na klabu yake ya Real Madrid pamoja timu ya taifa ya Croatia, ambayo ilicheza hatua ya fainali ya Kombe la Dunia na kufungwa na Ufaransa nchini Urusi mwezi Julai.

Modric mwenye umri wa miaka 33, ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA baada ya kupata asilimia 29.05 ya kura zilizopigwa, akifuatiwa na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ureno na klabu bingwa Italia, Juventus FC,  Ronaldo aliyepata asilimia 19.08 na Mohamed Salah wa timu ya taifa ya Misri na klabu ya Liverpool aliambulia asilimia 11.23.

Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, Modric alitoa shukurani kwa kila mmoja aliyemuwezesha kufikia hatua hiyo.

“Tuzo hii sio ya kwangu pekee yangu,” alisema. “Inapaswa kuhusishwa na wachezaji wenzangu wa timu ya taifa ya Croatia na klabu ya Real Madrid, ambao kwa pamoja wameniwezesha kufikia hatua hii kubwa katika maisha yangu ya soka. Mbali na wachezaji pia makocha wa pande zote mbili wanastahili tuzo hii, familia yangu nayo inapaswa kupewa heshima na kuthaminiwa katika tuzo hii,” aliongeza.

Kwa kudhirisha tayari nyota yake ilikua inang’aa kabla ya ushindi wa usiku wa kuamkia leo, Modric alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa fainali za kombe la dunia, na mwezi mmoja baadae alitajwa kuwa mchezaji bora wa barani Ulaya.

Wakati huo huo mshambuliaji kutoka nchini Brazil Marta alitangaza kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA mwanamke, akiwashinda wapinzani wake Ada Hegerberg na Dzsenifer Marozsan wote wa klabu ya Olympic Lyon ya Ufaransa.

Mohamed Salah alitangazwa kushinda tuzo ya bao bora la mwaka, kupitia bao alilolifunga wakati wa mchezo wa ligi ya England kati ya Liverpool dhidi ya Everton msimu wa 2017-18, akiwazidi wapinzani wake Gareth Bale na Cristiano Ronaldo.

Matokeo ya kura zilizopigwa upande wa mchezaji bora wa kiume; kwa asilimia:

  1. Luka Modric (29.05%)
  2. Cristiano Ronaldo (19.08%)
  3. Mohamed Salah (11.23%)
  4. Kylian Mbappe (10.52%)
  5. Lionel Messi (9.81%)
  6. Antoine Griezmann (6.69%)
  7. Eden Hazard (5.65%)
  8. Kevin De Bruyne (3.54%)
  9. Raphael Varane (3.45%)
  10. Harry Kane (0.98%)
Rais awashika mkono wafiwa, manusura MV Nyerere, walamba mamilioni
Video: Chadema haina hata Itikadi- Polepole