Huko Afrika ya Kusini nyuki wameingia kwenye injini ya ndege ya shirika la Mango na kusababisha kuchelewa kwa safari za ndege katika uwanja mkuu wa ndege mjini Durban.
Wataalamu wa nyuki waliitwa kuja kusaidia kuwaondoa nyuki hao karibu 20,000 kutoka kwa injini ya ndege hiyo.
Mmoja wa wataalamu hao amesema tukio hilo si la kawaida na kwamba huenda nyuki hao walikua wakipumzika kabla ya kuelekea mahali pengine.
Ameongeza kuwa hawakua na mpango wa kuishi ndani ya injini iliyo na ”harufu kali”.
Nyuki hao walijaa ndani ya injini ya ndege ya shirika la Mango chini ya dakika 25, hali ambayo ilisababisha ndege zingine tatu kuchelewa kuondoka katika uwanja wa Kimataifa wa King Shaka.
Msemaji wa shirika la ndege la Mango, Sergio dos Santos amesema ”Sijawahi kuona kisa kama hiki katika kipindi cha miaka minane niliyohudumu katika shirika la ndege”
Ilichukua muda kabla ya watalamu hao kuruhusiwa kuingia ndani ya uwanja wa ndege kwa sababu walihitaji idhini kutoka kwa mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege nchini.
Melvyn Dawson, mmoja wa wataalamu wa nyuki alisema ilikua ”kazi rahisi” na kwamba walichohitaji ruhusa tu ya kufikia ndege hiyo.
Akizungumza na shirika la habari la News24 Dawson, alisema, “Tumekumbana na visa kadhaa vya kuondoa nyuki waliyovamia mahali fulani lakini sijawahi kuona kisa kama hiki”.
Ameongeza kuwa nyuki hao wamehifadhiwa nyumbani kwa ndugu yake ambaye pia ni mfugaji nyuki na kwamba watapelekwa mashambani hivi karibuni.