Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amestaajabishwa na jinsi teknolojia ya asili ya nyuki ilivyotumika na Malkia Liti wa Singida katika kupambana na wakoloni, wakati alipotembelea Banda la maonesho ya Biashara la Mkoa wa Singida katika maonesho ya utamaduni aliyoyazindua jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika banda hilo, Waziri Mkuu alielezwa namna ambavyo mmoja wa machifu wa kale wa Wanyaturu, Malkia Liti alivyokuwa na uwezo wa kuwaamrisha nyuki kuwashambulia askari wa kikoloni na kuilinda himaya yake.
Ameambiwa kuwa, Malkia Liti aliweza kuitumia teknolojia hiyo kwa muda mrefu bila kupata madhara ya kushambuliwa au kukamatwa na wakolonii hadi pale alipokuja kusalitiwa na baadhi ya wasaidizi wake.
Kutokana na historia hiyo, na kwa heshima ya Malkia huyo uwanja wa michezo wa mkoani Singida ukabadilishwa jina kutoka kuitwa Namfua na kuwa Uwanja wa Liti kama moja ya utambuzi wa tamaduni za kuwaenzi waasisi wa kale.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipata maelezo hayo mara baada ya kuzindua Tamasha kubwa la Kitaifa la Utamaduni lililo na maonesho mbalimbali ya tamaduni ikiwemo ngoma, vyakula na historia mbalimbali za makabila ya nchini Tanzania.
Akizindua Tamasha hilo, Waziri Mkuu amesema walezi na wazazi wanatakiwa kuzingatia malezi ya watoto kwa kutenga muda wa kukaa nao ili kukemea suala la mmomonyoko wa maadili katika Taifa.
Amesema, vijana wote wa Kitanzania waache kuendekeza tabia ya kutumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii kwa kusoma au kuangalia mambo ambayo hayaongezi thamani ya maisha yao na badala yake watumie muda huo kufanya kazi.
“Ninaitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuongeza jitihada za kuandaa programu za elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kuthamini mila na desturi zetu na uzalendo, ili tutengeneze kizazi kinachozingatia maadili mema, tusikubali kamwe kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni,” amesema.
Ameongeza kuwa, jukwaa mojawapo ambalo Wizara hiyo inaweza kuanza nalo ni kuandaa mdahalo wa kitaifa kuhusu mmomonyoko wa maadili, utakaowapa picha halisi picha halisi ya hali ya maadili ilivyo nchini.
“Lakini jambo jingine ni kuunda kablu za maadili katika shule za Msingi na Sekondari, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa wana klabu ambazo zinawaelimisha wanafunzi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kwa hiyo na nyinyi Wizara kwa Kushirikiana na TAMISEMI igeni mfano huo mzuri,” alisisitiza Majaliwa.
Akizungumzia tamasha hilo, amesema “Naiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, iandae mwongozo wa jinsi gani matamasha haya yataendeshwa. Pia ninaiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na wadau ambao wanaandaa matamasha ya Utamaduni.“
Tamasha hili la kwanza kufanyika nchini, limeandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, limefanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kukutanisha mikoa 24 kati ya 26, kwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa jijini Mwanza Septemba 2021 wakati aliposimikwa uongozi wa kimila na kupewa jina la Chief Hangaya.