Nyumba za wabunge watatu wa vyama vya upinzani nchini Uganda ikiwa ni pamoja na ya mbunge ambaye ni mwanamuziki maarufu, Bobi Wine zimeripotiwa kushambuliwa kwa mabomu usiku wa manane.

Wabunge hao wameeleza kuwa matukio hayo yalitekelezwa kwa nyakati tofauti kati ya saa sita na saa saba usiku wa kuamkia leo, lakini wote wameeleza kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa au kupoteza maisha.

Bobi Wine ambaye hivi karibuni alikuwa mmoja kati ya wabunge walioshiriki katika kufanya vurugu bungeni kupinga kuwasilishwa kwa muswada wa kuondoa ukomo wa umri wa kugombea urais nchini humo, amesema kuwa mbali na mashambulizi hayo ya vilipuzi amekuwa akipokea vitisho vya kuua kila siku.

“Kwa mara ya pili, usiku wa jana vilipuzi vilitupwa tena kwenye nyumba yangu na viliripuka! Hakuna aliyeumia lakini mali ziliharibika,” Bobi Wine ameandika kupitia Twitter.

“Ningependa kuieleza dunia kuwa nimekuwa nikipokea vitisho vya kuua kila siku,” ameongeza kwenye tweet nyingine.

Mbunge mwingine, Allan Sewanyana alieleza kuwa vilipuzi vilirushwa karibu na chumba cha kulala cha mwanae lakini havikumdhuru.

Ahukumiwa mwaka mmoja jela kwa kumkashifu Rais Magufuli WhatsApp
JPM awataka wakurugenzi ‘waokoke’, kuvunja makundi