Aliyekuwa Mshambuliaji wa Ihefu FC, Mzambia, Obrey Chirwa anakaribia kujiunga na Kagera Sugar ili kuitumikia msimu ujao.
Chirwa aliyefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara msimu ulioisha huku akiwahi kuchezea timu za Azam FC na Young Africans ameshindwa kufikia makubaliano ya kuongezewa mkataba mpya hivyo kuamua kuondoka rasmi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Ally Masoud alisema ni kweli wapo baadhi ya wachezaji wako kwenye mazungumzo ya mwisho kuwasaini hivyo tuwe na subira.
Tumeanza kutoa mkono wa kwaheri kwa wale wote ambao hatutakuwa nao msimu ujao na baada ya hapo tutaanza rasmi kuwatangaza tuliowasajili, usajili wetu ni mzuri utakaoleta manufaa,” amesema.
Aidha Masoud alisema kikosi hicho tayari kimeanza maandalizi ya msimu mpya huku akieleza timu hiyo itaendelea kuweka kambi Mjini Bukoba na haitaenda Uganda kama ilivyokuwa mwaka jana.
Mbali na Chirwa, Kagera Sugar pia iko kwenye mazungumzo ya kupata saini ya mshambuliaji, Yacouba Sogne kutokea pia Ihefu baada ya mkataba wake kumalizika licha ya maongezi baina yao kuendelea.
Chirwa anaungana na Cleophace Mkandala aliyejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na matajiri wa Azam FC.