Mgombea Urais wa Kenya anaeungwa mkono na ngome ya NASA, Raila Odinga amepinga matokeo yanayoendelea kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEBC).
Akizungumza na waandishi wa habari saa chache zilizopita, Odinga amesema kuwa Tume haikufuata utaratibu wa kutangaza matokeo kwani wawakilishi wa vyama walio kwenye vituo hawakupewa fomu namba 34A ili wasaini matokeo yaliyotangazwa.
Odinga ameeleza kuwa kutokana na kutokuwepo fomu hizo ni vigumu kubaini matokeo yanayotangazwa na IEBC yanatoka wapi.
“Mfumo umeachwa na sasa ni mitambo ndio inayopiga kura. IEBC wamesema kwamba hakuna chama chochote kilichopinga matokeo. Lakini vyama vitapingaje matokeo bila kujua asili yake? Ni fomu namba 34A pekee inazoonesha chanzo cha matokeo,” amesema Odinga.
“Kwa hivyo, tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa kwa sasa na kuitaka tume ya IEBC itoe fomu 34A za kila kituo kabla ya matokeo zaidi kutangazwa,” aliongeza.
- Wizara ya Ardhi yabuni mbinu mpya za ulipaji kodi pango la ardhi
- Video: Kenyatta, Odinga mchuano mkali, Waliopiga mabilioni viwanda kitanzani
Hata hivyo, Msemaji wa Jubilee amesema kuwa madai ya NASA hayana mashiko kwani hakuna hakuna sehemu ambayo walishinda mwaka 2013 ambapo mwaka huu wameshindwa bali wamefanya vizuri pia kwenye maeneo ambayo walishindwa vibaya mwaka huo. Hivyo, aliwataka NASA kutoendelea kutoa maeneno aliyodai ni ya udanganyifu bali kujiandaa kukubali matokeo kwani itakayoshinda ni ‘Kenya’ na sio chama chochote cha uchaguzi.
Alisema kuwa fomu namba 34A iko katika mfumo wa kielektroniki hivyo yeyote akatayetaka kuichakachua ataonekana. Jubilee wanaonesha kuwa na uhakika wa kushinda katika uchaguzi huu ingawa matokeo yanaendelea kutangazwa huku zaidi ya asilimia 91 ya kura zote ikiwa imeshahesabiwa.
Tume imeendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi huo kwa njia ya matandao kama yanavyotoka katika vituo ambapo hadi sasa Kenyatta anaonekana kuongoza akiwa na asilimia 54.57 huku Odinga akiwa na asilimia 44.58. Wawili hao wanatofautina zaidi ya kura milioni moja.