Mwanasiasa mkongwe nchini Kenya, Raila Odinga atawania tena urais wa nchi hiyo kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2022, kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa chama chake, Seneta James Orengo.
Hii itakuwa mara ya tano kwa Odinga kuwania nafasi hiyo huku mara kadhaa akilalamikia rafu kwenye matokeo ya uchaguzi, na kufanya mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi uliopita 2017 kabla ya kubariki tena urais wa Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa marudio.
Hivi sasa, Odinga anaonekana kushirikiana kwa karibu na Rais Kenyatta katika kuwaunganisha wakenya na kuondoa uhasama.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya, Orengo pamoja na viongozi wengine waandamizi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) wamethibitisha nia ya Odinga kuwania tena nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa 2022.
Inaonekana dhahiri kuwa kama Odinga atawania nafasi hiyo, atachuana na William Ruto ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais, ambaye anaonekana kuwa na nguvu zaidi kwenye upande wa chama chake kuwania nafasi ya Urais mwaka 2022.
“Sio suala la kushangaza hata kidogo. Tunajua siku nyingi kuwa anajiandaa kwa ajili ya kugombea urais. Tuko tayari kumuunga mkono. Tunafanya kazi ya kuimarisha ngome yake,” Seneta Samson Cherargei anayemuunga mkono Ruto anakaririwa.
-
Sababu kwa nini nywele zako hazikui
-
Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta na Odinga waliwahi kueleza kuwa uamuzi wa kushikana mikono Machi 9 haukuwa na uhusiano wowote na suala la kutaka kuachiana madaraka mwaka 2022.
Kenyatta hatagombea tena nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba ya Kenya.