Klabu ya Brighton imekataa ofa ya pili kutoka kwa Chelsea kwa ajili ya kumnunua kiungo wa kati, Moises Caicedo.
Ofa ya hivi karibuni ya The Blues kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ecuador inaaminika kuwa inafikia karibu pauni milioni 70.
Caicedo aliomba kuondoka klabuni hapo Januari mwaka huu, huku Arsenal ikiwa na nia lakini Machi alisaini mkataba mpya hadi 2027.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye msimu uliopita aliwasaidia Seagulls hao kufuzu kucheza michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza na kufika nusu fainali ya Kombe la FA, bado anavutiwa na timu kadhaa za Ligi Kuu England.
Caicedo alijiunga na Brighton kutoka klabu ya Independiente del Valle ya Ecuador kwa kitita cha pauni milioni 4.5 Februari mwaka 2021 kabla ya kutolewa kwa mkopo kwa Beerschot ya Ubelgiji.
Alianza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Aprili 2022 na amecheza mara 53 wakati wake pale kwenye Uwanja wa Amex, akifunga mabao mawili.
Chelsea na Brighton zitamenyana Jumamosi hii mjini Philadelphia nchini Marekani katika mchuano wa kujiandaa na msimu mpya wa Ligi ya England unaojumuisha timu sita.