Katika hali isiyokuwa ya kawaida Ofisi ya Bunge imeshindwa kuteua wagombea wa vyama vya upinzani kwa ajili ya uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) unaotarajiwa kufanyika mapema hii leo.

Kushindwa kwa uteuzi huo kunatokana na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi huo ambapo Ofisi hiyo ya Bunge imevitaka vyama vya upinzani kurekebisha dosari zote zilizojitokeza.

Hayo yamesemwa na msimamizi wa uchaguzi huo Dkt. Thomas Kashililah, amesema kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Wananchi (CUF) havikuzingatia masharti ya Ibara 50 ya mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kutokana na upungufu huo msimamizi nimeshindwa kuteua wagombea wa kundi hilo, hivyo nmeviandikia vyama husika vyenye haki ya kugombea kurekebisha upungufu ulioanishwa,”amesema Dkt. Kashililah.

Aidha, kwa upande wake Ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene amesema kuwa hakuna utaratibu wowote uliokiukwa kwa kuteua wagombea wa EALA na kudai kuwa msimamizi wa uchaguzi kaamua kuja na utaratibu wake.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaaya amesema kuwa Chama hicho kina imani na Spika Job Ndugai kuwa atafuata sheria na Kanuni za uchaguzi.

Hata hivyo, uchaguzi huo unatarajiwa kutoa wabunge tisa watakao iwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki huku CCM ikitoa wabunge sita na watatu kutoka vyama vya upinzani.

 

Harrison Mwakyembe: Tuwekeze Kwa Vijana
Live: Bungeni Dodoma, Mkutano wa saba