Kiungo Mshambuliaji raia wa Nigeria, Nelson Okwa ametaja sababu za kushindwa kutamba akiwa na Simba SC, huku akimtaja aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa klabu hiyo  Zoran Maki.

Okwa ambaye ni kati ya wachezaji waliotemwa na Simba SC akiwamo kipa Beno Kakolanya aliyetangazwa jana (Juni 22) amesema maisha yake yalienda tofauti baada ya Maki kuondoka Simba SC, kwani ndiye aliyekuwa anamuamini na kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

“Nimeumia sana kuondoka katika kipindi ambacho sijakidhi mahitaji ya mashabiki na viongozi wangu, ila niseme tu nawashukuru kwa kuniamini katika kipindi chote nilichocheza hapa,” amesema Okwa.

Akizungumzia hatma yake baada ya kuondoka Okwa amesema, kwa sasa anaenda kupumzika kwanza kwao Nigeria, japo ana matumaini bado anaweza akarudi kucheza tena, nchini kama atapata ofa nzuri.

“Bado naipenda Tanzania na imani yangu ni kuona naendelea kucheza hapa, hadi sasa sijapokea ofa yoyote japo muda upo na lolote linaweza kutokea, tusubiri tuone itakuwaje,” amesema.

Okwa alitua Simba SC akitokea Rivers Utd ya Nigeria alianza vyema maisha katika timu hiyo kabla ya Zoran kutimka Septemba, 2022 na mambo kumtibukia.

Habari za uchunguzi kaa la moto Tanzania
Dkt. Tax afanya ziara Chuo cha Diplomasia Indonesia