Biashara iliyokuwa ikifanywa na Wawekezaji ya kununua vifaranga na Mayai kutoka nchi za nje imepigwa marufuku, baada ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, kusema kuwa Serikali haitaruhusu Mwekezaji yeyote kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au mayai ya kuku kutoka nchi za nje.
Ameyasema hayo Bungeni Mjini Dodoma, wakati wa maswali na majibu amesema kuwa katika kusimamia hilo kuanzia mwaka 2013 hadi 2017 vifaranga 67,500 vilivyoingizwa nchini kinyume na sheria viliteketezwa.
“Wapo wawekezaji wachache ambao hupewa vibali maalum vya kuingiza mayai au vifaranga vya kuku wazazi (Parent Stock) pekee na ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti uingizaji vifaranga na mayai unaendelea nchi nzima,”amesema Ole Nasha.
Aidha, ameongeza kuwa haiwezekani wawekezaji hao kwenda kununua Mayai na Vifaranga nchi za nje wakati hapa nchini vipo na kuna uwezekano mkubwa wa kuweza kuzalisha,
Hata hivyo, Amesema hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakaye kamatwa kwa kukiuka utaratibu uliowekwa na Serikali, hivyo watu wote wanaofanya biashara hiyo ikiwa ni pamoja na wawekezaji hao wanatakiwa kufuata taratibu na sheria za nchi.