Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amezipongeza halmashauri ya wilaya na Mji wa Njombe mkoani humo kwa kuendelea kupata hati safi kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.
Ametoa pongezi hizo wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya hiyo, lililoketi kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2017/2018 katika Halmashauri hiyo.
Amesema kuwa hatua hiyo Imetokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa watalaamu wa halmashauri hizo mbili, ambapo amezitaka halmashauri hizo kuendelea kudumisha ushirikiano huo na kuhakikisha mafanikio hayo yanaonekana pia kwenye miradi mingine.
Katika hatua nyingine Ole Sendeka amezitaka Halmashauri hizo kuhakikisha zinaendelea kupunguza hoja za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na waliosababisha uwepo wa hoja hizo wanapaswa kuchukuliwa hatua za Kisheria.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Joramu Hongoli amesema kuwa halmashauri hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wananchi kukosa huduma ya maji.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Valentino Hongoli amesema kuwa halmashauri hiyo kila mwaka imekuwa ikifanyiwa ukaguzi wa hesabu zake za Serikali na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Serikali.