Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amekanusha taarifa kuwa yeye ni mmoja kati ya wabunge wa CCM waliohamia Chadema wakimfuata waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Ole Sendeka amesema kuwa taarifa hizo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ni za uzushi na kwamba yeye hana mpango wa kukihama chama hicho.

“Nimesikia uvumi ambao ulikuwa unasambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba ama Christopher Ole Sendeka anakusudia kuhama Chama Cha Mapinduzi kwenda kwenye chama kingine cha siasa, au pengine ameshahama. Naomba niwahakikishieni kwamba sina mpango wa kukihama Chama Cha Mapinduzi,” alisema Ole Sendeka.

Mbunge huyo wa Simanjiro anaamini kuwa hakuna chama bora zaidi ya CCM hadi sasa. Pia amewashauri wale wote wanaokihama chama hicho kurudi kundini kwa kuwa huko waliko wanapoteza muda.

“Sijaona chama mbadala ambacho naweza kujiunga nacho. Naomba niwahakikishie kwamba chama hiki nina imani nacho, nina imani na uongozi ulipo sasa. Lakini zaidi nina imani na uongozi ulioteuliwa kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM. Huko kwingine, sioni matumaini yoyote kwa yeyote aliyekwenda huko. Pengine wanapoteza muda watarudi baadae kujiunga na chama hiki.”

Dk. Slaa Asema Anatishiwa Maisha, ‘Mapenzi Ya Mungu Yatimie’
Magoli Ya Mkono Yatawala Kura Za Maoni, Makamba, Ndugai, Nchemba Watajwa