Klabu ya AC Milan, imeweka sokoni jezi maalum za golikipa zenye jina la Olivier Giroud baada ya mshambuliaji huyo kuonesha ushujaa kama mlinda mlango kwenye mechi dhidi ya Genoa na kuisaidia AC Milan kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Giroud alilazimika kukaa golini baada ya golikipa Mike Maignan kutolewa nje kwa kadi nyekundu wakati Milan wakiwa wamemaliza idadi ya wachezaji watano wa mabadiliko.
Baada ya filimbi ya mwisho, wachezaji waliungana kusherehekea ushindi huo huku klabu ikimuongeza Giroud kwenye orodha ya kikosi chao kama golikipa, lakini pia kutengeneza jezi maalum zenye jina lake mgongoni.
Milan ilitoa taarifa kuwa: Usiku wa jana, Olivier Giroud alikua sehemu ya historia ya Milan kwa kuonesha ujasiri kwa kulinda lango katika dakika za mwisho kwenye mechi dhidi ya Genoa.
Klabu imeamua kuheshimu mchango wake kwa kumuweka kwenye orodha ya makipa, aidha, mashabiki sasa wanaweza kununua jezi maalum ya golikipa ikiwa na jina la Giroud 9′ kupitia maduka na tovuti rasmi ya klabu ya AC Milan.”
Rossoneri kwa sasa wako kileleni mwa Serie A, wakiwa na pointi 21, baada ya kushinda mechi saba kati ya nane za ligi hiyo.
Wapinzani wao wakubwa klabu ya Inter Milan, wanakamata nafasi ya pili wakiwa na pointi 19, huku Juventus wakija nafasi ya tatu wakiwa na alama 17.