Olivier Giroud ameweka wazi kuhusu mustakabali wa maisha yake huko Emirates Stadium, kwa kusema yu njiani kusaini mkataba mpya.
Giroud ambaye kwa sasa ni kama mkombozi wa kikosi cha Arsenal kufuatia hatua ya ufungaji wa mabao muhimu katika michezo iliyoshuhudia Arsenal wakihaha kusawazisha ama kusaka bao la ushindi, amemua kuweka wazi suala hilo kwa lengo la kuwaondoa hofu mashabiki wake.
Mkataba wa sasa wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, unatarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa msimu wa 2017-18.
Mashabiki wa Giroud wameingiwa hofu na kuhisi huenda mtu wao akawa njiani kuondoka Emirates Stadium, kutokana na tetesi zinazoendelea kuhusu usajili wa mshambuliaji wa Torino Andrea Belotti ambaye thamani yake ni Pauni milioni 56.
“Tupo katika hatua nzuri ya mazungumzo na wakati wowote tutafikia muafaka,” Giroud aliiambia tovuti ya Telefoot. “Ninataka kuendelea kubaki hapa ili niitimizie malengo Arsenal. Na bado ninajihisi furaha kuendelea kuwa sehemu ya kikosi.
Giroud alijiunga na Arsenal mwaka 2012, akitokea nchini kwao Ufaransa alipokua akiitumikia klabu ya Montpellier.