Mwendesha mashtaka mkuu nchini Sudan amesema kuwa kiongozi aliyeondolewa madarakani, Omar al-Bashir atafikishwa mahakamani wiki ijayo.
Mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo, Al Waleed Sayyed Ahmed amesema kuwa, Bashir anakabiliwa na mashtaka ya rushwa na kumiliki fedha za kigeni kinyume cha sheria.
Hayo yanajiri baada ya zaidi ya miezi miwili tangu jeshi lilipomwondoa Bashir madarakani kufuatia maandamano makubwa ya kitaifa yaliyopinga utawala wake.
Aidha, mwezi Aprili mwaka huu, mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alisema kuwa fedha zaidi ya dola milioni 113 zilikamatwa kutoka kwenye makazi ya al-Bashir.
Alisema kuwa polisi na wanajeshi na mawakala wa usalama walipata kiasi cha Euro milioni saba , Dola za Kimarekani 350,000 na Pauni za Sudan milioni moja.
Pia Ahmed amesema kuwa watuhumiwa wengine waliotumikia chini ya utawala wa Bashir bado wanachunguzwa, ingawa hakuwataja majina lakini alisema tuhuma dhidi yao ni kuhusu umiliki wa ardhi.
-
Omar al-Bashir kufikishwa kortini
-
Sudan kusini: Panga la kubana matumizi latua baadhi ya balozi kufungwa
-
Baraza la Kijeshi Sudan limekiri kuwashambulia waandamanaji
Omar al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi tarehe 11 Aprili baada ya maelfu ya waandamanaji wakiongozwa na muungano wa vyama vya watu stadi kupiga kambi mbele ya makao makuu ya jeshi katikati ya mji mkuu Khartoum kuanzia Aprili 6. Kwa sasa anazuiwa kwenye gereza la Kober.