Mkali wa RnB, Omarion ambaye usiku wa kuamkia leo aliwapa shangwe wakaazi wa jiji la Dar es Salaam kwa tamasha la aina yake, ameeleza siri ya kuamua kufanya miradi mingi ya muziki na Bosi wa WCB, Diamond Platinumz.

Msanii huyo wa Marekani ambaye aliingia nchini na kupokelewa na mwenyeji wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alisema kuwa kuna miradi mingi sana ambayo amefanya na Diamond kwa sababu ana ‘akili kubwa’.

“Nadhani sababu ni kwamba akili kubwa hufikiria sawa na nguvu kubwa hutafutana. Kwahiyo, siwezi kuvumilia kusubiri ngoma tuliyofanya pamoja, ni ngoma kali ya dunia ambayo itashika kona nyingi za sayari,” Omarion alifunguka.

Mkali huyo wa ‘Distance’ ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la B2K, aliacha kitendawili kwa mashabiki wa muziki, alipoulizwa kama Diamond pia atasikika kwenye albam yake mpya ya ‘Reasons’ inayosubiriwa na dunia.

Aliwataka mashabiki kuendelea kusubiri mengi kutoka kwake na Diamond, akisisitiza kuwa wamefanya miradi mingi mizuri na mikubwa.

Katika hatua nyingine, Omarion alisema kuwa aliamua kufanya video ya ‘Distance’ nchini Afrika Kusini kwa sababu Afrika ni Bara ambalo lina vitu vingi vya kipekee lakini watu wengi hasa wa Marekani hawajalitambua hilo.

Kolabo hiyo kubwa kwa Diamond imekuja siku chache baada ya kuanika mtandaoni vipande vya video ya wimbo aliofanya na Boss wa MMG, Rick Ross.

Matokeo ya Urais Kenya kutangazwa leo
Video: Sarkodie na Korede Bello wakutana kwenye 'Far Away'