Aliyekuwa Katibu Kiongozi wa Ikulu Tanzania na mwanadiplomasia, Ombeni Yohana Sefue ameteuliwa na kuwa Mtanzania wa kwanza kuwa kwenye jopo la watu mashuhuri kwenye mpango wa bara la Afrika wa kujitathmini kiutawala bora (APRM).

Jopo la watu mashuhuri ni chombo cha juu cha kuwashauri  wakuu wa nchi wanachama wa APRM kwenye uendeshaji kwenye kusimamia mpango mzima wa kujitathmini ambapo Wajumbe wa jopo hilo hudumu kwa miaka minne.

Akitoa taarifa za uteuzi huo Katibu mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib ambaye anahudhuria mkutano wa umoja wa Afrika Addis Ababa amesema Ombeni Sefue ameidhinishwa kwenye kikao cha juu cha Wakuu wa nchi za umoja wa Afrika ambao ni Wanachama wa APRM, ambapo chakato wa kuteua wajumbe hao huanzia kwenye kupendekezwa na nchi zao na baada ya mlolongo mrefu ambao una ushindani, majina ya waliokidhi vigezo hupelekwa mezani na kuidhinishwa na kikao cha juu cha APRM.

Aidha, Mwenyekiti wa Wakuu wa nchi APRM Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliwapongeza wajumbe wa jopo hilo na kuwataka washiriki vyema kuifanya APRM kuwa chombo chenye thamani Afrika kama Waasisi wake kina Benjamin Mkapa, Obasanjo na Thabo Mbeki walivyotarajia.

Wizara ya Maliasili na Utalii yamkingia kifua Prof. Maghembe
CCM: Chagueni viongozi wanaokubalika ili tuendelee kuongoza nchi