Ombi la Klabu Bingwa nchini Nigeria Rivers United la kutaka kuutumia Uwanja wa Adokiye Amiesimaka katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali dhidi ya Young Africans, limekataliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Rivers United itakuwa mwenyeji wa mchezo huo April 23, mjini Port Harcourt Nigeria, kabla ya kuelekea Dar es salaam-Tanzania kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa April 30.
Awali kabla ya Rivers United kuwasilisha ombi la mabadiliko ya Uwanja huko CAF, ilikuwa ikiutumia Uwanja wa Godswill Akpabio uliopo mji wa Uyo nchini Nigeria.
Rivers United waliandika barua hiyo, wakiomba kubadilishiwa uwanja na kurejea kwenye uwanja uliopo mjini kwao Adokiye Amiesimaka huko Port Harcort ambao umekataliwa na CAF.
Maamuzi hayo kutoka CAF, huenda yakawa na faida kubwa kwa Young Africans watakapokuwa ugenini Aprili 23, mwaka huu kucheza mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Robo Fainali.
Awali Rivers walikua wakiutumia Uwanja huu kwenye hatua ya makundi na baadae wakaomba kuruhusiwa kurejea.
Kwa mujibu wa mtandao wa CAF, uwanja huo waliouomba Rivers United haujakidhi viwango na hivyo watalazimika kuendelea kuutumia Uwanja wa Uyo Godswill Akpabio.
Uwanja huo ndio ambao ulitumika msimu uliopita kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Orlando Pirates (Afrika Kusini) dhidi ya RS Berkane (Morocco).
CAF kama wangeruhusu mchezo huo uchezwe kwenye Uwanja wa Adokiye Amiesimaka, basi wangepata ugumu kwani upo katika mji wao, hivyo ni lazima mashabiki wengi wangeingia kuwasapoti.
Ugumu mwingine ambao Young Africans watakaoukwepa ni hujuma ambazo wangezifanya nyingi Rivers United wangezifanya kama ilivyokuwa katika msimu uliopita walipokutana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.