Umoja wa Mataifa (UN) umeunda Kamati maalumu ya siri yenye wajumbe tisa kujadili mkanganyiko uliojitokeza kuhusu viongozi wa Serikali Afghanistan wanaopaswa kuhudhuria na kuhutubia Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) unaoendelea huko jijini New York nchini Marekani.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa kundi la wanamgambo wa Taliban wanaoongoza taifa la Afghanistan kuomba kuhutubia mkutano huo.
Taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa UN, Stephane Dujarric imesema tarehe 15 Septemba mwaka huu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Gueterres amepokea barua kutoka kwa Mwakilishi wa Serikali ya awali ya Afghanistan, Balozi Ghulam Isaczai iliyotaja viongozi waliopaswa kuhudhuria mkutano huo.
Amesema kuwa alipokea barua nyingine kutoka kwa Ameer Khan ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi iliyojiita Islamic Emirate of Afghanistan yaani Afghanistan akiomba kushiriki katika mkutano huo.
Katika barua hiyo, Waziri huyo alidai serikali ya awali iliyokuwa chini ya Rais Ashraf Ghani imeondolewa madarakani hivyo moja kwa moja mwakilishi wa Afghanistan huko UN yaani Balozi Isaczai hatambuliki kama mwakilishi wa nchi yao
Hata hivyo, Msemaji huyo amesema kamati maalumu ya siri yenye wajumbe tisa itakaa kujadili mkanganyiko huo ili kupata jawabu la mwakilishi sahihi wa Afghanistani.
Itakumbukwa Uongozi mpya wa Afganistan ambao ulingia madarakani tarehe 15 Agosti, 2021, hautambuliki kama mwakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, ratiba ya kikao cha kamati hiyo haijapangwa licha ya kwamba Afghanistani imepanga kuhutubia mkutano hup tarehe 27 Septemba.