Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz sasa anaendelea vizuri kiafya tofauti na siku chache zilizopita ambapo mitandaoni taarifa zilisambaa zikitaka watanzania kumuombea kwani alilazwa ICU (Intensive Care Unit) huko nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu mara baada ya madaktari kugundua kuwa alikunywa sumu iliyodhuru mfumo wake wa kupitisha chakula.
Ommy Dimpoz amefunguka kuwa amekuwa akisumbuliwa na mfumo wake wa kupitisha chakula ambapo taarifa toka kwa madaktari bingwa zilionesha kuwa koo la kupitisha chakula limeziba hali iliyompelekea kushindwa kumeza chakula wala maji.
Ommy amesema kwa mara ya kwanza alipotembelea hospitali moja hapa nchini Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi kubaini tatizo, walibaini kuwa anakansa hali ambayo ilimtisha na kumfanya achukue hatua zaidi kubaini ukweli wa tatizo hilo.
Hata hivyo Ommy alifanikiwa kufika hospitali moja nchini Mombasa na kufanyiwa vipimo na kumkatia rufaa Afrika kusini ambapo walibaini kuwa ametumia sumu iliyoathiri mfumo wa chakula, hivyo alifanyiwa upasuaji na kuwekewa mfumo bandia wa chakula.
”Wakanichana sasa kwenye tumbo mpaka karibia na kifua na wakanichana hapa kwenye shingo kwahiyo wakavuta ytumbo juu hjalafu wakaunganisha wenyewe wanavyojua kwenye utaalamu wao ili ityenegeneza njia moya kwahiyo ile njia ya zamani ikawa imekufa” amesema Dimpoz.
Ameongezea kuwa ilikuwa oparesheni kubwa ya kufa na kupona, lakini anamshukuru Mungu zoezi hilo limemazilika salama na sasa anaona Nuru.
Aidha Ommy amesema hadi sasa hafahamu ni katika mazingira gani alikunywa sumu hiyo kwani kwa akili zake timamu na kumbukumbu zake hajawahi kutumia sumu ya aina yeyote ametoa shukrani zake za dhati kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa sala na dua zao, sasa yupo katika mapumziko akirejea afya yake ataendelea kufanya kazi yake ya muziki kama kawaida.