Rasmi Uongozi wa Simba SC umefanisha DIli la usajili wa Kiungo Mshambuliaji wa Klabu ya Rayon Sports ya nchini Rwanda, Leandre Willy Onana kwa Dola za Marekani 80,000 sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 189.5.

Simba SC imemalizana na kiungo huyo baada ya tetesi nyingi kuzagaa za timu hiyo kuwepo katika mipango ya kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.

Onana ametua Simba SC huku akiacha kumbukumbu nchini Rwanda ya kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya nchini humo msimu huu 2022/23, akifunga mabao 16 na sasa anachukua nafasi ya Mghana, Augustine Okrah.

Imefahamika kuwa Onana kabla ya kusajiliwa na Simba SC, alipata ofa kadhaa kutoka nchini Morocco, Dubai pamoja na Young Africans kabla ya kubadili gia na kumfuata Mkongomani Fabrice Ngoma aliyevunja mkataba klabu ya Al Hilal ya Sudan.

Mmoja wa mabosi wa Simba SC, kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, amesema kiungo huyo alisaini mkataba huo wa miaka miwili juzi Jumapili usiku ikiwa ni muda mfupi baada ya kutua nchini na kufichwa katika moja ya hoteli kubwa ya Jijini Dar es salaam.

Bosi huyo amesema kuwa tofuati na dau hilo la usajili, kiungo huyo atachukua mshahara wa Dola za Marekani 6000 sawa na Shilingi Milioni 14.2 kwa mwezi kwa kipindi cha miaka miwili atakachokuwepo Simba SC.

Ameongeza kuwa kiungo huyo mara baada ya kusaini Jumapili (Juni 11), alibakia nchini hadi juzi Jumatatu huku akitarajiwa kurejea nyumbani kwao kukamilisha taratibu nyingine.

“Onana alikuja nchini wikiendi na kusaini mkataba usiku wake akiwa na Meneja wake Karenzi (Alex) a aliyeongozana naye kutoka Rwanda na kuja hapa nchini Tanzania.

“Taratibu zote za usajili zimekamilika za Onana kusaini mkataba huo wa miaka miwili, ambao yeye amekubali kusaini kuichezea Simba SC katika msimu ujao ambao tumepanga kufanya vizuri.

“Usajili wake unakuwa wa kwanza ndani ya Simba SC wakati dirisha kubwa la usajili likisubiriwa kufunguliwa kusuka kikosi imara kitakachokuwa tishio msimu ujao.

“Kwa sasa hatuwezi kuachia picha kwa kuwa kuna vitu kidogo tunakamilisha na baada ya hapo ndio tutaanza kuachia picha za wachezaji wetu mmoja baada ya mwingine,” amesema bosi huyo

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amezungumzia hilo la usajili na kusema kuwa: “Tayari yapo majina ya wachezaji ambao kocha wetu Roberthino (Roberto Oliviera) na kilichobakia ni kupewa mikataba pekee na uzuri pesa ipo ya usajili.”

Simba SC imepanga kukiboresha kikosi chao kwa kufanya usajili bora na kisasa ili kuhakikisha wanafanikisha malengo yao ya msimu ujao ni kufika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na kurudisha mataji ya Michuano ya Tanzania Bara.

Arsenal yakaribia usajili wa Declan Rice
Vinicius akabidhiwa namba ya kazi Real Madrid