Mshambuliaji kutoka nchini Cameroon na Klabu ya Simba SC Willy Esomba Onana amesema amewasikia wote wanaomchambua na sasa wataona mziki wake atakaporejea Dimbani mwezi Septemba.
Onana alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Rayon Sports ya Rwanda, amezua mijadala mitandaoni tangu aanze kucheza nchini Tanzania, ambapo baadhi ya watu wanaamini aina yake ya uchezaji inaigharimu timu yake, huku wengine wakimponda kwa kusema anacheza ‘soka laini.”
Kufuatia shutuma hizo Onana amesema amewasikia mashabiki na wadau wanaojadili aina yake ya uchezaji, hivyo kwa sasa anayafanyia kazi yote aliyoyaona na kuyasikia kutoka kwao, na ameahidi kurejea akiwa moto zaidi na kuiwezesha Simba SC kupaa zaidi katika Michuano yote wanayoshiriki.
“Nimesikia na nalifanyia kazi, najua Simba ina mashabiki wengi wanaoipenda sana timu yao. Hivyo wanachokitaka ni kuona wachezaji wao na timu inafanya vizuri,” amesema Onana, mwenye bao moja kwenye Ligi Kuu na kuongeza;
“Nipo hapa kutimiza malengo ya klabu. nitajitahidi kufanya kila linalowezekana ili tufikie kile tulichokipanga kukifanya msimu huu, naamini mashabiki watafurahi na mambo yatakuwa mazuri timu itakaporejea kwenye michuano mbalimbali.” amesema.
Onana na Mcameroon mwenzake, Che Fondoh Malone walimekuwa wakifanya mazoezi ya ziada mara kadhaa kwa pamoja lakini pia wamekuwa sambamba na timu kwenye mazoezi ya jumla.
Simba SC itarejea uwanjani tena kwenye mechi za kimashindano, kati ya Septemba l5-17, itakapocheza mechi ya mkondo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, ikianzia ugenini.