Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ameyataka Mataifa Ulimwenguni kuondokana na wasiwasi wa tishio la maafa ya kimataifa juu ya matumizi ya Nyuklia, na kusema wote wanatakiwa wajitolee kuilinda amani iliyopo na si kuhofia kwani hali hiyo itawafanya wasifikiri juu ya maendeleo.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Septemba 26, 2022, hafla iliyofanyika huku mjadala wa kila mwaka wa Baraza kuu ukifikia ukomo, katika Ukumbi wa Baraza Kuu.
Amesema, “Silaha za nyuklia ndizo nguvu za uharibifu zaidi kuwahi kuundwa. Hazileti usalama wowote , ni mauaji na machafuko tu na kuondolewa kwa vikwazo kungekuwa zawadi kuu tunayoweza kutoa kwa vizazi vijavyo.”
Guterres, pia amekumbushia kwamba, “Niweke wazi enzi ya vitisho vya nyuklia lazima iishe na wazo la kwamba nchi yoyote inaweza kupigana na kushinda vita vya nyuklia limepotoshwa, utumiaji wowote wa silaha ya nyuklia utaturudisha nyuma.”
Hata hivyo, amesisitiza haja ya kuwa na maono mapya ya kutokomeza silaha za nyuklia, akiashiria ajenda yake mpya ya amani inayotoa wito wa kupokonya silaha na kuendeleza uelewa wa pamoja wa vitisho vingi, vinavyoikabili jumuiya ya kimataifa.
Wakati mjadala wa Baraza Kuu ukimalizika, Katibu Mkuu huyo pia ametoa wito kwa nchi wanachama kuondoka New York na dhamira mpya ya kufanya kazi kwa mustakabali wa amani kwa kusema, “bila ya kuondoa silaha za nyuklia, hakuwezi kuwa na amani, uaminifu na hakuwezi kuwa na mustakabali endelevu.”