Afara Suleiman – Babati.
Baadhi ya Wananchi Wilayani Babati Mkoa Manyara, wametoa maoni yao kufuatia ongezeko la Kodi ya jengo kwa nyumba ya kawaida ambayo ni Shilingi 18,000 kwa mwaka, ambapo awali ilikuwa 12,000 na kwa sasa itamlazimu mpangaji kulipa shilingi 1,500 kwa mwezi tofauti na bei ya awali iliyokuwa shilingi 1,000.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wananchi hao wameiomba serikali kuwatafutia au kuwawekea utaratibu wa ulipaji Kodi kulingana na hadhi ya Nyumba, kwani baadhi zimekosa huduma ya umeme au maji na hivyo viwekwe viwango stahiki.
Aidha, wamesema pia Serikali iangalie kwa jicho la pili namna ya kupunguza utitiri wa Kodi kwa Wananchi, kutokana na uhalisia wa hali ya ugumu wa maisha na upandaji wa gharama za mahitaji muhimu unaowakabili, ili kuleta uhueni kwao na jamii nzima kiujumla.
Hata hivyo, mmoja wa wananchi hao Hawa Rashidi akizungumza Kwa niaba ya wenye nyumba amesema ni vyema Serikali kabla ya kuongeza Kodi iwashirikishe baadhi ya wadau, ili kuondoa migongano baina ya wapangaji na wenye nyumba.