Kupitia hotuba yake kwa njia ya Luninga, Rais wa mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno ametangaza hali ya hatari kutokana na mafuriko ambayo yanaathiri zaidi ya watu milioni moja katika nchi hiyo, huku akisema umoja katika ushughulikiaji wa janga hilo utawezesha mamlaka kudhibiti maafa.
Huku karibu nusu ya jiji ikiwa chini ya maji, wakaazi wa N’Djamena wanatumia mitumbwi yao kuondoka katika maeneo yaliyofurika na Serikali inasema imeweka mpango wa kutoa makazi, chakula, na vyoo, lakini watu wengi bado wana mashaka na kufanikiwa kwa mpango huo na kuokoa maisha ya wengi.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, linasema ingawa sehemu nyingi za za Chad, zinakabiliwa na mvua kubwa kila mwaka, lakini kwa mwaka huu hali ni tofauti kwani mvua inayonyesha haina mfano wake, na madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi.
Maeneo yaliyoathiriwa zaidi yako kusini mwa nchi hiyo, yakijumuisha mikoa 18 kati ya 23 iliyopo nchini humo ambayo mingi imekumbwa na maafa huku Rais Deby Itno akitoa wito wa usaidizi wa kiufundi na kifedha kutoka kwa washirika na Mataifa.
Mito iliyofurika imeharibu zaidi ya hekta 470,000 za mazao na ardhi ya kilimo na kufanya watu wengi kuwa na hofu ya uhaba wa chakula au hali hiyo kupelekea baa la njaa ambapo kwa mwezi Juni, Chad ilitangaza dharura ya chakula na Umoja wa Mataifa ulikadiria mwaka jana kuwa watu milioni 5.5 wa Chad au zaidi ya theluthi moja ya watu walihitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.