Ili kutoa nafasi kwa Vijana kujifunza misingi ya ndoa na kuielewa kabla ya kuingia kwenye ndoa, Kamati za kupinga vitendo vya Udhalilishaji Zanzibar, zimeshauri kuundwa kwa mfumo utakaotoa elimu ya ndoa itakayofundishwa katika ngazi mbalimbali za Taasisi za Elimu.

Ushauri huo, umetolewa wakati wa kikao kilichoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, kupitia mradi wa kutumia Jukwaa la Habari Kupambana na vitendo vya udhalilishaji unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la kimataifa la maendeleo ya Denmark, DANIDA.

Kikao hicho cha kuwasilisha ripoti ya miezi mitatu ya ufuatiliaji na utoaji wa elimu ya kupinga vitendo hivyo katika jamii, pia kilieleza ukosefu wa mfumo huo unapelekea Vijana wengi kuingia kwenye ndoa bila kupata elimu ya kutosha ya ndoa jambo linalosababisha kuongezeka kwa talaka zisizokuwa za lazima.

Wamesema, hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la migogoro ya familia na kupelekea ndoa nyingi kuvunjika jambo ambalo linasababishwa na ukosefu wa elimu ya utambuzi wa misingi kabla, huku Afisa Mradi, Zaina Salum akiwahimiza wanakamati kushirikiana kwa ukaribu kufuatilia matukio ya udhalilishaji na kutoa elimu kwa jamii.

Awali, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kati, Ali Sheha alisema katika Wilaya hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kumeripotiwa kesi saba za kutelekezwa, malezi kesi tatu, kubaka kesi tatu, Shambulio la kuumiza mwili kesi moja ambapo chanzo kikubwa cha kesi hizo ni matokeo ya utelekezaji uliotokana na migogoro ya ndoa.

Kwa upande wake Afisa Jinsia Wilaya Mangaribi A Unguja, Dodo Rajab Ismail amesema licha ya Ofisi ya Mufti kuchukua juhudi za kuanzisha madarasa maalum ya kutoa elimu ya ndoa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maimamu, bado haitoshi kuwajengea Vijana utambuzi wa misingi ya ndoa.

Amesema, “Ili kukabiliana na hili tatizo la ongezeko la talaka, tunahitaji kuwepo madarasa maalum ya kufundisha masomo ya ndoa kwenye skuli na madrasa ili vijana wajifunze kwa undani masuala ya ndoa na sio kupata mafunzo hayo pale tu wanapotaka kuingia kwenye ndoa.”

Katika hatua nyingine kamati hiyo ambayo inaundwa na maafisa kutoka idara mbalimbali za serikali ngazi ya wilaya wakiwemo Dawati la kijinsia Jeshi la Polisi, Usitawi wa jamii, mkono kwa mkono, mahakama, waratibu wa kupinga ukatili pamoja na viongozi wa dini walisema ipo haja ya jamii kurudi katika malezi ya pamoja waliolelewa wazee hali iliyosababisha vijana kukuwa katika maadili mema.

Naye Afisa jeshi la Polisi kituo cha Mwera, Wilaya ya Magharibi A, Jamal Himid Hassan alieleza kuwa, “suala la talaka tujiangalie sisi wazazi kwanza tuko sawa.? Lazima tubadilike, wazazi wengi sasa hivi tumekuwa waongo na wanafiki, kila mmoja hakubali kosa la mtoto wake hata kama mtoto kakosea.”

Mkutano huo, uliwashirikisha wajumbe kutoka Wilaya Tano za Unguja ikiwemo Kusini, Kaskazini A &B, Kati, Magharibi A, iliyogundua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii za muhali uliopitiliza, mlolongo wa kesi katika vyombo vya maamuzi, baadhi ya wazazi kuwafanya watoto wao mtaji na ushirikano mdogo wa wazazi katika malezi na makuzi ya watoto.

John Terry kuibukia Saudi Arabia
Azam FC kumng'oa John Noble Tabora