Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Nchi za Afrika wanachama wazalishaji wa zao la Kahawa kuwekeza zaidi katika kupata vifaa na mashine za kisasa za uchakataji wa zao hilo, ili kuongeza thamani ya kahawa kabla ya kuuzwa nje ya bara hilo.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa Barani Afrika wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda.
Amesema, ili kuinua sekta hiyo ni muhimu sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali kuweka msisitizo katika kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuwekeza katika vifungashio borahuku akiwasihi wakulima wa zao hilo kujikita katika kilimo bora na cha kisasa ili sekta hiyo iwe na mchango kwa wananchi na uhifadhi wa mazingira.
Aidha, Makamu wa Rais pia amesema licha ya bei ya kahawa kuwa na mwenendo mzuri kwa kipindi kirefu bara la Afrika limeendelea kubaki nyuma kwa kuwa na asilimia 12 tu ya uzalishaji Duniani, huku mwelekeo katika ukanda huo ukiendelea kupungua kwa kasi.
Amesema ni muhimu kutatua changamoto zilizopo na kuchukua hatua kuhakikisha fursa ya uzalishaji kahawa inatumika vema kwa kuzingatia kuongezeka kwa bei ya zao hilo duniani na uwepo wa soko la watu bilioni 1.4 lililopo Afrika.