Beki kutoka nchini Kenya Joash Onyango Achieng ameonesha kuyakubali mazoezi ya Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Seleman Matola, ambaye alikua na jukumu la kukinoa kikosi cha klabu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021.
Matola alikabidhiwa jukumu la kuliongoza benchi la ufundi, siku moja baada ya aliyekua Kocha Mkuu wa Simba SC Sven Vannderbroek kuthibitika amesitisha mkataba wake, na kutimkia nchini Morocco kujiunga na F.A Rabat.
Onyango amesema kwa kipindi chote walichofanya kazi na Matola wakiwa kisiwani Unguja-Zanzibar mambo yalikua mazuri, na ndio maana walipata matokeo ya kufurahisha kabla ya kupoteza kwa changamoto ya mikwaju penati dhidi ya Young Africans kwenye mchezo wa fainali jana Jumatano (Januari 13).
“Maandalizi yalikua mazuri, ninampongeza kocha Matola kwa kufanya kazi yake kama ilivyotarajiwa, hakika yeye amekua kiongozi imara na alisaidia kuwa na furaha katika michezo iliyopita, tuliopata matokeo hadi kufika fainali.”
“Kocha Matola ni rafiki wa kila mchezaji, na hiyo ilikua rahisi kwake kufanya kazi kwa weledi mkubwa katika kipindi chote tukiwa hapa Zanzibar, kwa hakika nimefurahishwa sana na kazi yake kama Kaimu Kocha Mkuu.” Amesema Onyango
Baada ya mchezo dhidi ya Young Africans Joash Onyango alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, kufuatia kuonesha kiwango bora na imara hasa katika safu ya ulinzi ya Simba SC ambayo ilikua ngumu kupitika.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021 ilifikia tamati jana usiku, kwa kikosi cha Young kuibuka mabingwa kwa kuwabanjua Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kwa changamoto ya mikwaju ya penati nne kwa tatu.
Timu zilizoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu 2021 kutoka Zanzibar ni Jamhuri, Chipukizi, Malindi FC na Mlandege, huku Young Africans, Simba SC, Namungo FC na Azam FC zikitokea Tanzania Bara.