Beki wa kati kutoka Kenya Joash Onyango Achieng amekataa kuthibitisha taarifa za kuomba kuondoka Simba SC mwishoni mwa msimu huu, baada ya taarifa hiyo kusambaa katika Mitandao ya kijamii.
Tangu juzi Jumanne (Mei 09) Onyango amekuwa akitajwa kukutana na Uongozi wa Simba SC na kuutaka usimuweke kwenye mipango ya msimu ujao, kwa sababu anahitaji kuondoka.
Beki huyo amesema taarifa za yeye kuondoka ama kubaki Klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, zinapaswa kuulizwa kwa viongozi wa Simba SC, ambao amedai wana nafasi nzuri ya kutoa ufafanuzi.
“Siwezi kuzungumza chochote kuhusiana na suala hilo kama lipo viongozi ndiyo watu sahihi wa kulizungumzia, lakini mimi siwezi kuwa na jibu kuhusiana na mambo ambayo yamekuwa yakizushwa na watu.” amesema Onyango
Hata hivyo alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, kuzungumzia hilo, amesema: “Sina taarifa hiyo rasmi kutoka kwa uongozi, tusubirie muda ukifika tutaweka wazi.”
Tangu atue nchini, Onyango ameisaidia timu yake kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, Ngao ya Jamii na kufika Robo Fainali katika Michuano ya CAF mara tatu.
Beki huyo amekuwa akicheza kwa mafanikio katika kikosi cha kwanza hadi sasa ni mchezaji ambaye ana uhakika wa kuanza sambamba na Henock Inonga.