Wamiliki wa vyuo binafsi vya kada ya famasi nchini, wametakiwa wasibadilishe vyuo vikawa kama biashara, kwani serikali inatarajia kupata wataalamu watatoa huduma zinazostahili kwenye vituo vyakutolea huduma za afya nchini.
Wito huo umetolewa na Msajili wa Baraza la Famasi, Elizabeth Shekalaghe ofisini kwake jijini Dodoma.
Shekalaghe amesema kuwa kila mwaka idadi ya vyuo inaongezeka. Amesema hadi sasa baraza hilo limeidhinisha vyuo 52 ngazi ya cheti hadi diploma, ambavyo tayari vimesajiliwa na NACTE. Hivyo,alisema lazima kuwe na wataalamu wenye uwezo ambao wanaendana na mahitaji ya sasa.
“Kama Baraza la Famasi tunao wajibu wa kusimamia kwa umakini vyuo ili kuhakikisha ubora wamafunzo yatolewayo iendane na mitaala na mahitaji kulingana na hali ya sasa” amesema.
Shekalaghe amesema idadi ya wataalamu wa kada ya Famasia, imekua ikiongezeka ingawa si kwa kasikubwa ndani ya miaka miwili, Baraza limesajili wafamasia 2,111.
Kwa upande wa fundi dawa sanifu, Shekalaghe amesema ndani ya miaka miwili iliyopita baraza hilolimesajili wataalamu wa kada hiyo 365 na hivyo kuwa na mafundi dawa sanifu 3,040 nchini.
“Upande wa fundi dawa sanifu kwa mwaka huu tumesajili wapatao 694, kada hii bado inahitajika ilikuweza kusimamia utoaji wa dawa kwenye vituo licha ya kwamba bado wanaendelea na mafunzo ngazi ya stashahada” amesema.