Nahodha na Mshambulaiji wa Mabingwa wa Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ kwa Wanawake ‘Simba Queens’ Opa Clement, ameushukuru Uongozi wa Simba SC kwa kufanikisha maandalizi ya kikosi chao, kuelekea Michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Simba Queens imepata nafasi ya kushiriki Michuano hiyo, baada ya kutawazwa kuwa Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ mwezi Agosti, wakiifunga SHE Coperates ya Uganda.
Opa ametoa shukurani hizo katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Jumanne (Oktoba 25) jijini Dar es salaam, uliotoa taarifa za safari ya Simba Queens kuelekea Morocco, kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Opa amesema: “Tunawashukuru viongozi wetu kwa sapoti kubwa wanayotupatia, wamekuwa wakiweka mazingira yetu ya kazi kuwa rahisi, kikubwa tunawaomba mashabiki waendelee kutuombea ingawa hawatakuwepo uwanjani.”
“Tunafahamu michuano itakuwa migumu lakini lengo letu ni kuhakikisha tunafika Nusu Fainali.”
Katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake Simba Queens imepangwa ‘Kundi A’ na wenyeji AS FAR (Morocco), Green Buffaloes (Zambia) na Determine Girls (Liberia).
Simba Queens itaanza Kampeni ya kusaka taji la Afrika Oktoba 30 kwa kucheza na wenyeji AS FAR (Morocco), kwenye Uwanja wa Moulay Hassan, mjini Rabat.
Mabingwa Watetezi Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) wamepangwa ‘Kundi B’ sambasamba na timu za Bayelsa Queens (Nigeria), Wadi Degla (Misri) na TP Mazembe (DR Congo).