Mkurugenzi wa huduma za kinga, wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Dkt. Leonard Subi ameagiza mikoa yote nchini kuendesha oparesheni maalumu za ukaguzi wa sehemu kuuzia chakula, nyumba za kulala wageni, mabucha, masoko na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009.
Lakini amewatahadhalisha maofisa afya kutotumia nguvu au kudai rushwa wakati wa kufanya ukaguzi huo.
Dkt. Subu ametoa maagizo hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma, lengo likiwa ni kuboresha hali ya usafi wa mazingira nchini ili kuepusha magonjwa ya mlipuko.
Aidha ameagiza vyombo vya usafiri, mabasi, meli, majahazi, bajaji vikaguliwe ili kubaini uzingatiaji wa usafi wa vyombo hivyo na upulizaji dawa ya kuua wadudu ufanyike na cheti maalumu cha kuthibitisha ukaguzi kitolewe.
” Vyombo ambavyo vitabainika kuwa na uchafu uliokithiri visiruhusiwe kutoa huduma na pia vitozwe faini kwa mujibu wa sheria ya afya ya jamii” amesema Dkt. Subu.
Pia ameagiza ufanyike ukaguzi wa kaya kwa kaya maeneo yote nchini na hatua stahiki zichukuliwe kwa watakaobainika kwenda kinyume cha kanuni za afya ikiwemo matumizi ya vyoo bora, udhibiti wa taka ngumu, maji taka na usafi wa mazingira.
Vilevile amewataka wamiliki wote wa majengo ya biashara ya vyakula wahakikishe wanasajiliwa na Baraza la Afya Mazingira kwamujibu wa sheria namba 20 ya mwaka 2007.