Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kununua tiketi zote za viti vya mzunguko kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ili kutoa nafasi kwa mashabiki kuingia bure kushuhudia mchezo wa pili kundi E kuwania kusaka tiketi ya kufuzu kombe la Dunia, timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itakapowakaribisha Morocco Jumanne Novemba 21,2023
Stars itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na ari zaidi baada ya kuanza kwa ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Niger na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo Gerson Msigwa amekabidhi zawadi ya shilingi milioni 10 kwa kikosi hicho ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia ya kununua kila bao kwa mechi ambazo kikosi hicho kitaibuka na ushindi.
Msigwa amesema Serikali itaendelea kutoa hamasa kwa kikosi hicho kuhakikisha inafikia malengo ya kufuzu kwa mara ya kwanza fainali za kombe la Dunia.
Kwa upande wake nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono na kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu hiyo kwenye mchezo wa Jumanne dhidi ya Morocco
Mchezo huo utapigwa majira ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, muda uliopangwa na FIFA maalum kwaajili ya kutoa fursa kwa mashirika yenye haki za matangazo ya TV kwa watazamaji wa ukanda wa Afrika Magharibi ambao kwao itakuwa ni saa mbili usiku.