Mshambuliaji wa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23 USM Alger Tumisang Orebonye amesema kuwa licha ya kuwa wao kumefanikiwa kuwa Mabingwa lakini Young Africans ni timu bora zaidi kuwahi kukutana nayo msimu huu.
Orebonye raia wa Botswana amesema Young Africans walikuwa bora sana kwenye mechi zote mbili walizokutana ila imekuwa kama bahati zaidi kwao kuweza kuwa mabingwa na kuongeza kuwa hata timu hiyo ya Tanzania ilistahili kuwa mabingwa.
Mshambuliaji huyo ambaye ameweka rekodi ya kuchukua kombe hilo mara mbili mfululizo akiwa na timu mbili tofauti za RS Berkane na sasa USM Alger amesema kiungo cha Young Africans kiliwavuruga zaidi kwenye mechi ya mwisho.
“Young Africans ni timu bora sana, wana wachezaji wazuri kwenye kila eneo, walicheza vizuri wakiwa kwao na walicheza vizuri zaidi wakiwa ugenini. Siyo kazi rahisi kutufunga USM Alger tukiwa kwenye uwanja wetu.
“Nafikiri sisi tulikuwa na bahati zaidi na ndiyo maana tumekuwa mabingwa na ilipaswa kuwa hivi kati yetu sisi wawili kwamba lazima mmoja awe bingwa, lakini ni bora sana hawa hasa kwenye eneo la kiungo lilikuwa bora sana,” amesema.