Oscar Garcia ametangazwa kuwa meneja wa kikosi cha klabu ya St Etienne kinachoshirtiki ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa (Ligue 1), baada ya kutimuliwa kwa Christophe Galtier aliedumu klabuni hapo kwa miaka minane.
Mwishoni mwa msimu wa 2016/17, uongozi wa St Etienne uliafiki kwa pamoja kumtimua Galtier, baada ya kuwa na msimu mbovu.
Garcia anajiunga na klabu hiyo akitokea FC Salzburg ya nchini Austria, na anabebwa na sifa ya kutwaa ubingwa wa nchi hiyo mara mbili mfululizo. Sifa nyingine kwa meneja huyo kutoka Hispania, ni kutwaa mara mbili ubingwa kombe la chama cha soka cha Austria mara mbili.
Aliwahi kuwa meneja wa klabu za England kama Watford na Brighton & Hove Albion, na kisha alitimkia nchini Israel kukinoa kikosi cha Maccabi Tel Aviv.
“Wasifu wa Oscar Garcia unajitosheleza. Ni mshindani, amethibitisha hilo kwa kazi yake nzuri aliyoifanya akiwa na Salzburg, tunaamini ataweza kufanikisha mpango wa kukinyanyua kikosi chetu kuanzia msimu ujao wa ligi ya Ufaransa.” Amesema rais wa St Etienne Romeyer alipohojiwa na tovuti ya klabu hiyo. (www.saintetienne.com)
St Etienne ilimaliza katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ya Ufaransa msimu uliopita, na alitolewa kwenye michuano ya Europa League kwa kufungwa na Manchester United kwenye hatua ya 32 bora.