Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ametoa wito kwa wamiliki wa sehemu za kazi wa mkoa wa Mwanza kuipokea na kuitekeleza ipasavyo kampeni ya kutokomeza ajali na magonjwa katika sehemu za kazi ya Vision Zero.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa katika hafla ya kuzindua kampeni hiyo kwa mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi, amesema endapo wamiliki wa sehemu za kazi watapata mafunzo ya uhakika kuhusu utekelezaji kampeni hiyo, ni dhahiri kuwa uzalishaji utaongezeka na kuleta tija kwa serikali na wananchi wote kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya kutoa semina kuhusu utekelezaji wa kampeni hiyo kwa waajiri hao ambao ni wanachama wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mkurugenzi wa Mafunzo, Tafiti na Takwimu wa OSHA, Joshua Matiko, amesema kupitia kampeni hiyo wataendelea kuwaelimisha waajiri ili waweze kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya na usalama wa wafanyakazi wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Mwanza, Dkt. Elibariki Mmari, amesema wanachama wake wameipokea vizuri kampeni ya Vision Zero na wanashiriki katika mafunzo ili kutambua wajibu wao katika utekelezaji wa kampeni hiyo.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wameeleza kufurahishwa kwao na kampeni ya “Vision Zero” na kuahidi kupeleka mrejesho katika taasisi zao ili kuanza utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa OSHA, Kanda ya Ziwa, Mjawa Mohamed, amesema wataendelea kutoa elimu na kufanya uhamasishaji zaidi katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.
Dhana ya “Vision Zero” ilibuniwa na Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi za Jamii Duniani (ISSA) na inatekelezwa na nchi mbali mbali duniani kwa namna fofauti kutegemeana na mazingira ya nchi husika.