Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi – OSHA, imefanya semina elekezi kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mkoani Arusha, ikilenga kutoa uelewa kwa Kamati hiyo kuhusu majukumu yanayotekelezwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, amesema masuala ya usalama na afya ni mtambuka na yanagusa sekta zote za uchumi, hivyo ni vyema kushirikiana kuimarisha mifumo ya usimamizi wa usalama na afya kwa wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sillo Baran ameishukuru OSHA kwa mafunzo hayo ambayo yamewajengea uelewa mzuri kuhusu masuala ya usalama na afya. Pia ameitaka OSHA kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wafanyakazi nchini ili kuleta tija katika maeneo ya kazi.
Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru kamati hiyo kwa kuishauri vyema serikali kuhusu masuala ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi na amewahakikishia ofisi hiyo itaendelea kusimamia kwa ufanisi masuala hayo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema taasisi hiyo itahakikisha ustawi wafanyakazi unaimarika sambamba na kulinda uwekezaji kupitia mifumo ya usalama na afya.
Aidha, Semina hiyo pia ilieleza namna taasisi hiyo iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inavyosimamia masuala ya Usalama na Afya katika sehemu za kazi.