Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich wanahusishwa na mpango wa kumsajili Mshambuliaji kutoka nchini Nigeria na klabu ya SSC Napoli ya Italia Victor James Osimhen.
Osimhen amekuwa gumzo katika mipango ya usajili wa Barani Ulaya majira ya Kiangazi, kufuatia kukiwasha kisawasawa katika Ligi Kuu ya Italia na Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu huu 2022/23.
FC Bayern Munich inakuwa sehemu ya klabu kubwa Barani humo zilizotajwa kumuwania Osimhen, na kama itaingia rasmi katika mbio hizo itakabiliwa na upinzani mkubwa wa usajili wa Mshambuliaji huyo.
Osimhen amefanikiwa kufunga mabao 21 akiwa na SSC Napoli msimu huu ndani ya Serie A, na ndiye kinara ufungaji katika klabu hiyo yenye maskani yake mjini Naples.
Msimu uliopita, Osimhen alitajwa kuwa Mchezaji Bora mdogo wa Ligi ya Italia ‘Serie A’ msimu uliopita 2021/22, na sasa anaipambania timu yake kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Imeelezwa kuwa, Osimhen huenda akarejea Bundesliga na kuonesha ubora wake kwani awali alishindwa kufanya hivyo akiwa VfL Wolfsburg kuanzia 2017 hadi 2019.