Mshambuliaji wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Ousmane Dembele amekanusha kuwa katika harakati za kuihama klabu hiyo na kutimkia England kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajli baadae hii leo.
Dembele ambaye mwishoni mwa juma lililopita alikua jijini London kuitikia mualiko wa baadhi ya wachezaji wa Arsenal, amesema safari yake jijini humo haikuwa na uhusiano wowote wa kuanza harakati za kusajiliwa na The Gunners kama ilivyoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, amekiri kuwa na urafiki wa karibu na baadhi ya wachezaji wa Arsenal, na kuonekana kwake jijini London, kulidhihirisha ukaribu huo, lakini amesisitiza kuendelea kuwa mchezaji wa FC Barcedlona kwa msimu wa 2018/19.
Amesema kwa sasa ameshaanza mazoezi na kikosi cha Barca, kwa ajili ya mchezo wa Spanish Super Cup ambao utachezwa mwishoni mwa juma hili kwenye uwanja wa Ibn Batouta, mjini Tangier-Morocco, huku mwamuzi Carlos del Cerro Grande akipewa jukumu la kusimamia sheria 17 za mchezo wa soka siku hiyo.
“Nitaendelea kuwa Barcelona, na nipo tayari kwa mapambano ya msimu ujao, licha ya kukabiliwa na changamoto ya kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza.”
“Ninajiandaa na mchezo wa Spanish Super Cup, nina uhakika wa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza mchezo huu, hivyo niwaondoe shaka mashabiki wa Barca kuhusu uvumi unaoendelea kunihusu, katika kipindi hiki cha usajili.” Alisema Dembele
Dembele ambaye alikua miongoni mwa wachezjai waliounda kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa wa dunia nchini Urusi mwezi uliopita, anahusishwa na mpango wa kusajiliwa kwa mkopo na klabu ya Arsenal ya England.