Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Ousmane Dembele amewasilisha maombi ya kutaka kuondoka FC Barcelona, kupitia dirisha dogo la usajili, ambalo litafunguliwa rasmi mwezi Januari 2019.
Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa hana maelewano mazuri na meneja wa mabingwa hao wa Hispania Ernesto Valverde kwa madai ya kuwa na utovu wa nidhamu, amethibitisha kuwasilisha ombi la kutaka kuondoka, alipozungumza na mwandishi wa tovuti ya Goal jana jumapili.
Mshambuliaji huyo amesema anaamini mwezi Januari ni wakati mzuri wa kuondoka FC Barcelona, baada ya kuwa na changamoto za hapa na pale, ambazo hakuwa tayari kuzitaja, licha ya kuhusishwa na sakata la utovu wa nidhamu.
“Nimewasilisha ombi la kutaka kuuzwa mwezi Januari, ninaamini uongozi wa Barca utalikubali, ninahitaji uhuru wa kucheza soka langu, kuna mambo mengi nyuma ya pazia, ambayo sipaswi kuyaweka hadharani,”
“Ninachokwambia kwa sasa nimewasilisha ombi la kutaka niuzwe mwezi Januari, hayo mengine kuhusu sababu zinazo nisukuma hadi kufikia hatua hii, tambua ni changamoto za kawaida katika mchezo wa soka.’ Alisema Dembele.
Dembele ambaye aliifungia bao la kusawazisha FC Barcelona katika mchezo wa La Liga mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Atletico Madrid, ameanza kuwaniwa na klabu za Arsenal na Liverpool zote za England.
Mbali na klabu hizo za England, pia mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG), nao wanahusishwa kwenye kinyang’anyiro cha saini ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21.
Hata hivyo PSG wanahusishwa kwenye mpango huo, huku ikisemekana huenda wakamtumia mshambuliaji wao kutoka nchini Brazil Neymar ambaye anapigiwa chepuo la kurejea Camp Nou, ili kumpata kwa urahisi Dembele.
Dembele bado hajaonyesha uwezo wake kisoka tangu alipotua FC Barcelona akitokea Borussia Dortmund mwaka 2017, na haijafahamika nini kinachomsibu hadi kufikia hatua ya kuonyesha utovu wa nidhamu.
Usajili wake uliigharimu FC Barcelona Euro milioni 105 sawa na dola za kimarekani milioni119.01, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na mshambuliaji kutoka Neymar, aliyetimkia PSG.