P-Funk Majani ametoa rai yake kwa Mfalme wa Rhymes, rapa mkongwe Afande Sele akimtaka kumshika mkono Harmorapa katika safari yake ya muziki.
Majani ametoa kauli hiyo kupitia Planet Bongo ya East Africa Radio, baada ya kutakiwa kuzungumzia alichowahi kueleza Afande Sele kuwa aliamua kuahirisha kutoa wimbo wake wenye ujumbe baada ya kuona maandishi ya mtayarishaji huyo nguli kwenye kundi moja la ‘WhatsApp’ akieleza kuwa muziki wenye ujumbe hivi sasa hauna nafasi zaidi ya burudani.
Ilielezwa kuwa kwa mujibu wa Afande Sele, Majani alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akimtambulisha Harmorapa kwenye ulimwengu wa muziki, huku akimpa nafasi zaidi kama mburudishaji.
Hata hivyo, P-Funk alisema kuwa huenda Afande Sele hakumuelewa vizuri alipozungumzia nyimbo za ujumbe huku akiweka wazi kuwa ‘amezimiss’ sana nyimbo zenye ujumbe lakini wakati huu soko linaendeshwa na nyimbo za burudani.
“Kuna era ya sasa hivi imetokea watu wanaimba vitu-vitu tu, mapenzi zaidi na clubbing.. ujingaunjinga tu. Ila kuna wengine bado wanaweka ujumbe hapa na pale lakini ujumbe hauna nguvu kama zamani,” alisema Majani.
“Kingine ningependa kumwambia Afande Sele kama anasikiliza, kama umeona dogo labda anapwaya ama anayumba katika sanaa yake, kuwa kaka yake, muandikie mashairi, msaidie, mshike mkono, wape muongozo hawa vijana kwa sababu wewe ni Mfalme wa Rhymes,” aliongeza.
Mtayarishaji huyo mkongwe wa Bongo Records, hivi karibuni alilitambulisha rasmi kundi lake jipya la Bongolos huku akitambusha pia kazi mpya ya Harmorapa iliyopewa jina la ‘Nundu’.