Ukiitaja Bongo Fleva, Bongo Records na P-Funk Majani ni majina ambayo yatakuwa yakisafiri na wewe kwenye simulizi la uasisi wa muziki huo, hivyo mtayarishaji huyo akitoa ‘nondo’ kwa wasanii na wadau ni muhimu kuzipigia mstari na kuzifanyia kazi.
Majani ambaye amewahi kuweka historia ya kuwa na asilimia 100 ya nyimbo zote alizotengeneza kwenye chati za muziki za redio karibu zote nchini, miaka zaidi ya kumi na tano iliyopita, amewataka wasanii kuhakikisha wanasoma na kuelewa sheria zinazohusu sanaa ili kulinda haki zao bila kuingilia haki za watu wengine.
‘The Super Duper Producer’ kama alivyoitwa na wengi, amesema kuwa tangu alipoanza kusoma sheria za sanaa na kuzungumza na wanasheria, ameongeza uelewa mkubwa na kutambua jinsi ya kudhibiti haki zake zisiibiwe huku akichora mstari wa kuzingatia haki za kila mmoja anayefanya naye kazi.
“Kama wewe ni msanii usiwe mvivu na usiwe ignorant (mjinga). Jaribu kujifunza sheria za muziki na kujua mfumo wa muziki sahihi unaendaje, kabla hujaanza kulalamika na kuongeaongea maneno mengi, fahamu haki zako kama wewe ulichokifanya na fahamu haki za wenzio walichokifanya,” ameiambia Clouds Media Group.
Gwiji huyo wa midundo amewataka wasanii kutokurupuka wanapotaka kudai haki zao bali kufanya utafiti na kujiridhisha kama ilivyokuwa kwa Mwana FA na AY ambao mwaka jana walishinda kesi dhidi ya kampuni ya simu.
“Usikurupuke tu kwa kufahamu kuwa kama umetumbukiza sauti kwenye wimbo au kama umetengeneza tu beat (mdundo) basi wewe ndio unayeumiliki,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Majani amefunguka kuwa ukimya wake unatokana na kukata tamaa kwani sanaa ya muziki nchini imekuwa haimtendei haki, licha ya kuwekeza muda na fedha zake kwa kipindi kirefu akizipa mafanikio nyimbo nyingi na wasanii wengi.
“Nimekata tamaa kwa namna moja au nyingine, mimi mchango wangu ni mkubwa. Bongo Fleva hii mimi ndiye nimeijenga, kuileta kwenye biashara ni mimi. Nimewekeza sana muda wangu, fedha yangu lakini kipato kurudi hakuna,” alisema.
Nikukumbushe tu kuwa Majani ndiye Mtayarishaji wa Muziki aliyeweka rekodi ya msanii wake Juma Nature kuwa wa kwanza kuujaza ukumbi wa Diamond Jubilee, kwenye uzinduzi wa albam yake ‘Ugali’ na kisha kufanya shows kwenye viwanja kama Kirumba jijini Mwanza akiitambulisha albam hiyo.
Ni Majani huyuhuyu aliyepika albam ya marehemu Ngwair iliyobatizwa jina la ‘Aka Mimi’, inayotajwa kuwa kati ya albam tano nzito za muda wote za Bongo Fleva. Kwenye orodha hiyo ya albam tano za muda wote lazima utazitaja ‘Ugali’ ya Juma Nature, ‘Machozi Jasho na Damu’ ya Profesa Jay, ‘Aka Mimi’ ya Albert Mangwea na mbili utakazozikumbuka zaidi.