Imeelezwa kuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba SC Pablo Franco Martin amewasilisha maombi kwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Stars, Kim Poulsen na shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ kuwaomba awaondoe wachezaji saba wa Simba kwenye kambi ya Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Ombi la Kocha huyo kutoka nchini Hispania, limedaiwa kuwa na sababu kubwa moja la kutaka kuwa na wakati mzuri na wachezaji wake katika kipindi hiki cha kujiandaa na mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN ya Niger.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa April 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili kufikisha alama 10 zitakazowavusha hadi Robo Fainali.
Kocha Mkuu Taifa Stars Kim Poulsen alitaja kikosi chake Juma lililopita huku akiwaita wachezaji saba wa Simba SC, ambao asilimia kubwa wanacheza kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Pablo.
Wachezaji wa Simba SC waliotajwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Kibu Denis.
Hata hivyo hadi sasa hakuna jibu lolote kutoka kwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars na Shirikisho la soka nchini Tanzania ‘TFF’ kuhusu kukubaliwa ama kukataliwa kwa ombi hilo.
Taifa Stars ilianza kambi mwishoni mwa juma lililopita jijini Dar es salaam ikijiandaa na mchezo wa kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati utakaochezwa leo Jumatano (Machi 23) Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku.
Stars pia itacheza michezo mingine miwili ya Kimataifa ya kirafiki dhidi ya Botswana Jumamosi (Machi 20) na Sudan Jumanne (Machi 29) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Stars inajiandaa na Michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ sambamba na Fainali za Mataifa Bingwa Afrika ‘CHAN 2024’.