Klabu ya Singida Fountain Gate FC inatarajia kumtangaza kocha wake mkuu Jumamosi (Oktoba 14), huku majina ya makocha wa zamani wa Simba SC, Pablo Franco Martin na Didier Gomes da Rosa, yakitajwa ni miongoni mwa makocha waliotuma wasifu wao kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mjerumani Ernst Middendorp.
Awali, uongozi wa Singida Fountain Gate FC kupitia kwa Rais wa klabu hiyo, Japhet Makau, alitangaza kabla ya kukutana na Simba SC wangemtangaza kocha huyo anayekuja kukinoa kikosi cha timu hiyo, lakini ratiba imebadilika kutokana na taratibu za kiutawala.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Masanza, amekiri kuwa walikuwa na mpango wa kumtambulisha kocha mapema kabla ya kucheza na Simba SC, lakini mazungumzo bado hayajakamilika na wanaendelea kupitia CV (wasifu) za makocha wengi.
Amesema Gomes na Pablo ni miongoni mwa makocha zaidi ya 100 walituma CV zao na wako katika mazungumzo kuangalia ni kocha yupi anaweza kuwafikisha katika malengo.
“Tumekuwa na majadiliano na makocha mbalimbali, tunahitaji kupata kocha ambaye atakuwa juu na si timu kuwa juu yake, tunatarajia hadi juma hili tutamtangaza kocha wetu awe Gomes au Pablo hilo litajulikana siku hiyo.
“Tunahitaji hadi Tunapokwenda Ruangwa, Lindi kucheza dhidi ya Namungo FC Kocha Mkuu ameshapatikana na tumemtangaza rasmi kuwa sehemu ya benchi la ufundi,” amesema Massanza.
Kuhusu kikosi, amesema wachezaji wamepewa mapumziko ya siku tatu, na kesho Alhamis (Oktoba 12) wataingia kambini kujiandaa na mechi yao ijayo dhidi ya Namungo FC.
“Ninaimani baada ya kurejea wachezaji ambao hawako kwenye majukumu ya timu ya taifa, wataingia kambini na tunatarajia kutafuta timu ya kucheza mechi moja ya kirafiki kwa kipindi cha siku 10 timu inapokuwa kambini,” amesema Massanza.
Singida Fountain Gate FC wanatarajia kusafiriki kwenda Ruangwa, Lindi kukabiliana na wenyeji wao, Namungo FC Oktoba 22, mwaka huu, kwenye dimba la Majaliwa, mkoani humo.