Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin amefunguka mazingira magumu waliyokutana nayo wakiwa nchini Niger, kwa ajili ya Mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Simba SC ilikua ugenini mjini Niamey Jumapili (Februari 20), kucheza mchezo huo dhidi ya Mabingwa wa Niger USGN na kulazimisha matokeo ya sare ya 1-1.
Kocha Pablo amesema wachezaji wake walikutana na hali ngumu wakiwa Niger kiasi cha kushindwa kupumua vizuri kutokana na hali mbaya ya hewa.
Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema haikuwa kazi rahisi kwao kupata alama moja dhidi ya wenyeji wao, kwani kila kitu kwao hakikuwa rafiki, mbali na hali mbaya ya uwanja kwenye sehemu ya kuchezea, hata hali ya hewa ilikuwa tatizo.
“Wachezaji wangu wanapaswa kupongezwa sana kwa kile walichopata tukiwa Niger, kulikuwa na mazingira magumu sana, hali ya hewa ilikuwa mbaya sana kiasi cha wachezaji kupumua kwa tabu.”
“Uwanja hasa eneo la kuchezea hapakuwa rafiki hata kidogo, kila kitu kilikuwa kigumu. Lakini wachezaji waliungana na kuipambania timu yao.” Amesema Kocha Pablo
Simba SC itaendelea na kampeni yakusaka alama tatu nyingine za ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika siku ya Jumapili (Februari 27), kwa kucheza na RS Berkane nchini Morocco.
Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ ikifikisha alama 4, ikifuatiwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 3 sawa na RS Berkane ya Morocco, huku USGN ikishika mkia wa Kundi hilo kwa kumiliki alama Moja.