Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin amekubali kupoteza mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika jana Jumapili (Februari 27), dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Simba SC ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 2-0, na kuporomoka kutoka nafasi ya kwanza hadi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D ikiendelea kusalia na alama 04, huku RS Berkane ikifikisha alama 06.
Kocha Pablo amesema kupoteza mchezo huo ni sehemu ya mapambano ya kuwania nafasi ya kutinga Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho, hivyo anarudi Tanzania kujipanga na mchezo ujao dhidi ya RS Berkane utakaopigwa Machi 13, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hata hivyo Kocha huyo amesema hana budi kujivunia umahiri uliooneshwa na wachezaji wake katika michezo miwili ya ugenini, huku wakirejea Tanzania na alama moja kufuatia sare ya 1-1 walioipta dhidi ya USGN Februari 21.
“Tumepoteza lakini katika michezo mitatu tumekuwa timu pekee ambayo ilipata alama ugenini.”
“Tuna michezo miwili nyumbani, malengo yetu kwa sasa ni kushinda michezo hiyo na kujaribu kutafuta alama ugenini.” amesema Kocha Pablo.
Mabao ya RS Berkane yalikwamishwa wavuni na Adama Ba na El Bahri dakika ya 32 na 41.