Mshambuliaji wa Borussia Dortmund Paco Alcacer amesema hana cha kujutia, baada ya kuondoka kwa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona mwishoni mwa msimu uliopita.
Alcacer ambaye alijiunga na BVB kwa mkopo wa miaka miwili, amesema tangu alipotua nchini Ujerumani maisha yake yamekua ya tofauti, na kila mwishoni mwa juma amekua akipata nafasi ya kucheza.
Amesma lengo lake kubwa lilikua ni kucheza soka kila mwishoni mwa juma na sasa mipango hiyo imetimia, hivyo hana nafasi ya kufikiria alipotoka na kuanza kujutia hatua ya kuondoka kwake FC Barcelona.
“Ukweli siku zote umekua ukitumika kama ufunguo ya mafanikio, nimesema ukweli wangu wa moyoni, siwezi kujutia lolote kuhusu kuondoka FC Barcelona.”
“Ninafurahia sana maisha ya hapa, lengo langu lilikua ni kucheza soka kila mwishoni mwa juma, leo ninafurahia hali hii, na mahusiano mazuri na wachezaji wenzangu pia ni chagizo lingine la kunogesha maisha yangu hapa Ujerumani.” Alisema mshambuliaji huyo alipohojiwa na televisheni ya Borussia Dortmund.
“Nimejifunza mengi nilipokua na FC Barcelona, nimecheza na wachezaji wenye uwezo mkubwa kama Lionel Messi, Luis Suarez na wengine, hilo ninajivunia sana, leo ninatumia ujuzi nilioupata kufanya kazi katika klabu yangu mpya.”
Alcacer mwenye umri wa miaka 25, alilazimika kuondoka FC Barcelona kufuatia kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza tangu alipoajiriwa meneja Ernesto Valverde msimu wa 2017/18.