Kiungo kutoka nchini Ivory Coast na Klabu ya Young Africans, Pacome Zouzoua, ameshusha presha ndani ya kikosi hicho baada ya awali kupata majeraha ya bega, lakini sasa yupo fiti, huku mwenyewe akiahidi kuipambania timu hiyo katika michezo iliyosalia ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D.
Pacome ambaye aliiokoa Young Africans katika mchezo dhidi ya Al Ahly kwa kufunga bao la kusawazisha Jumamosi (Desemba 02), ni sehemu ya wachezaji wachezaji wa klabu hiyo waliosafiri mapema leo Jumanne (Desemba 05), kuelekea nchini Ghana kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi D.
Pacome amesema anauchukulia kwa umuhimu mkubwa mchezo ujao ugenini dhidi ya Medeama watakaocheza huko Ghana, akiamini ushindi ndio utakaowarejeshea matumaini ya timu hiyo kufuzu hatua inayofuatia ya Robo Fainali.
Pacome amesema wamepanga kushinda michezo yote iliyobaki, kwa kuanza dhidi ya Medeama, licha ya ugumu wa mchezo huo, kwao wachezaji wamekubaliana kla mmoja kucheza kwa kujituma ili wafanikishe malengo yao.
“Tunakibarua kigumu cha kuhakikisha tunafuzu hatua inayofuatia ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kama yalivyokuwa malengo yetu msimu huu.
“Kwangu binafsi nitahakikisha ninaipambania timu yangu, katika michezo iliyopo mbele yetu kuhakikisha tunapata pointi tisa ambazo ninaamini zitatupeleka Robo Fainali.
“Ninataka kuona ninacheza katika kiwango bora katika michezo hiyo, kwa kuanzia huu uliokuwepo mbele yetu dhidi ya Medeama ambao watakuwepo nyumbani kwao, lakini hiyo haituzuii sisi kufanikisha malengo yetu ya ushindi,” amesema Pacome.
Young Africans imesaliwa na mechi nne za hatua ya makundi, dhidi ya Medeama (ugenini na nyumbani), kisha CR Belouizdad (nyumbani), watamaliza na Al Ahly ugenini.
Kwa sasa Young Africans ina alama moja, inashika nafasi ya mwisho katika Kundi D, huku Al Ahly wakiongoza wakiwa na pointi nne, Medeama na CR Belouizdad, zote zina pointi tatu.