Kiungo Mshambuliaji fundi wa Young Africans, Pacome Zouzoua amesema kuwa wamejifunza baada ya kipigo kutoka Ihefu FC, lakini watarudi wakiwa katika kiwango bora kuelekea michezo inayofuatia.
Young Africans juzi Jumatano (Oktoba 04) ilikutana na kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Higland Estates, Mbarali Mkoani Mbeya.
Katika mchezo huo, Young Africans ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Pacome huku ya Ihefu yakipachikwa na Lenny Kissu na Charles Ilanfya.
Baada ya kuwasili jijini Mwanza tayari kwa mchezo wa kesho Jumamosi (Oktoba 07), Pacome amesema kuwa kipigo hicho ni somo kwao wachezaji, hivyo watarejea imara katika michezo inayofutia.
Pacome amesema kuwa kocha wao Muargentina Miguel Gamondi wameona upungufu uliosababisha wapoteze mchezo huo huku akiamini atafanyia maboresho ili mchezo wao wapate ushindi.
“Katika soka kufungwa ni lazima, ngumu timu kupata ushindi katika kila mchezo, na bila kufungwa mpira wa miguu usingekuwa na mvuto.
“Kwetu wachezaji tumejifunza kupitia hili, na tutarudi tukiwa vizuri katika michezo ijayo ya ligi inayofutia na kikubwa ni kupata ushindi pekee,” amesema Pacome.